Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Yawakutanisha Wadau wa Utafiti Nchini

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekutanisha Wadau wa shughuli za Utafiti nchini ili kujadili kwa pamoja namna bora ya kuboresha taratibu na mifumo mbalimbali inayotumika kusajili Tafiti nchini. Hii ni pamoja kutafakari uratibu unaoelewana kwa lengo la kutimiza azma ya kitaifa na kuongeza ufanisi kwa pamoja, ikiwemo kuboresha mifumo na maudhui vitakavyokuwa jumuishi na shirikishi kwa kuziunganisha Taasisi zinazojihusisha na *usajili na uratibu wa Taasisi au shughuli zinazohusiana na* Utafiti nchini, Mkutano huo umefanyika tarehe 28 Februari 2022 katika Ofisi za Makao Makuu ya COSTECH zilizopo Sayansi - Kijitonyama, Jijini Dar es salaam.

Mkutano huo ulilenga kujibu changamoto zinazojitokeza mara kwa mara hususani za usajili wa Tafiti. Utofauti wa mifumo na kukosekana kwa uelewa wa pamoja kwa mfumo wa Kitaifa unaounganisha Wadau wa Tafiti nchini kutoka Taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

Aidha, wadau kwa pamoja wamekubaliana kuanzisha mchakato wa mazungumzo Ili kuhakikisha wanaongeza ushirikiano ya pamoja na kuongeza tija katika mawasiliano ya karibu ili kuwarahisishia watafiti upatikanaji wa taarifa na kufuata taratibu zilizoratibiwa vizuri ikiwemo usajili wa tafiti na vibali kwa miongozo iliyoboreshwa ya kufanya utafiti nchini.

COSTECH imeratibu mkutano huo kupitia Mwaliko wa Mkutano wa Wadau wa Utafiti, akihitimisha Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt Amos Nungu, amesisitiza majadiliano na kuongeza ushirikiano wa wadau kwa ajili ya kutambua na kutatua kwa pamoja changamoto zinazoikabili tasnia ya utafiti ndiyo njia pekee za kuharakisha maendeleo nchini.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alisema uratibu wa tafiti ni sehemu ya utekelezaji wa Jukumu la Tume kwa kuzingatia vipaumbele vya Utafiti vya Kitaifa.

Mkutano huo umehudhuriwa na wadau wa shughuli za Utafiti nchini akiwemo Msajili wa Asasi za Kiraia (NGO’s), Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Taasisi ya Utafiti wa Wanyapori Tanzania (TAWIRI), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Idara ya Uhamiaji Tanzania.


PICHANI: Wadau wa shughuli za Utafiti nchini waliokutanika kujadili kwa pamoja namna bora ya kuboresha taratibu na mifumo mbalimbali inayotumika kusajili tafiti nchini, uliofanyika katika ukumbi ndani ya Jengo la COSTECH, Sayansi – Kijitonyama, Jijini Dar es salaam.