Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Yazindua Program ya OFAB kwa Mwaka wa 2022

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa Semina kwa waandishi wa habari za Kisayansi kufuatia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip I. Mpango kuzindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 mnamo tarehe 12 Februari, 2022 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Sera hiyo mpya inalenga kutoa matokeo chanya kwa kusimamia kazi ya uhifadhi wa mazingira nchini.

Akifungua semina hiyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Bugwesa Katale alisema kuwa ni shauku ya Tume kuona watanzania wanaelimishwa juu ya sera mpya ya Mazingira.

“Ndugu waandishi kama mnavyofahamu COSTECH majukumu yake makubwa ni kuendeleza na kuratibu shughuli za Sayansi na Teknolojia hapa nchini, tunafanya hivi kwanza kwa kufadhili utafiti pamoja na Ubunifu, tunaandaa miongozo mbalimbali kwaajili ya Utafiti na Ubunifu na vilevile tunandaa vipaumbele vya utaifiti vya Taifa; na kubwa zaidi tunalolifanya ni Kuishauri Serikali katika masuala ya Sayansi na Teknolojia " Dkt. Bugwesa alisema

Dkt. Bugwesa aliongeza kuwa kabla ya Sera hii mpya kulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa mwongozo wa kisera wa usimamizi wa matumizi ya bioteknolojia ya kisasa. Teknolojia hii ina matumizi mbalimbali ya viwanda, afya, mazingira na kilimo.

Aidha akizindua semina hiyo Dkt. Bugwesa alisema kuwa hapo awali kulikuwa na sheria na miongozo mbalimbali iliyokuwa inasimamia bioteknolojia, na sera ya kisekta kama sera ya taifa ya kilimo ya mwaka 2013, sera ya taifa ya mifugo ya Mwaka 2006 na sera ya taifa ya bioteknolojia 2010.

Hivyo basi Tume kwa kuona umuhimu wa Sera Mpya ya Mazingira imechukua jukumu la kualika wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano (Mazingira) na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ili wajibu maswali ambayo waandishi wamekuwa wakiyaelekeza kwa Tume kufuatia uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Bw. Anjelist Lujuo akihitimisha semina hiyo aliwashukuru wataalamu kwa kutoa elimu kupitia mawasilisho yao na kujibu maswali yote na kutoa wito kwa waandishi wa habari kuwafikishia umma wa watanzania habari zilizosahihi.

Kaimu Mkrugenzi Mkuu wa COSTECH , Dkt. Bugwesa Zabron Katale (aliesimama katikati) na  Bw. T. Chali (kushoto) kutoka Ofisi ya Makamu wa Raisi, Muungano na Mazingira pamoja na Bw. Tumbuko - OFAB Meneja Ofisi za Nairobi