COSTECH Yaendelea Kutoa Elimu kwa Watafiti na Waandishi wa Habari Jijini Arusha

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inaendelea kutoa elimu kupitia mafunzo ya uandishi wa habari za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na kutoa rai kwa waandishi wa habari na watafiti nchini.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia(COSTECH), Dk.Philbert Luhunga Jumanne ya tarehe 15 Machi, 2022 katika Ukumbi  wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha uliopo Jijini Arusha.

"Ndugu zangu warsha hizi za kuwakutanisha waandishi wa habari pamoja na watafiti zilianza muda mrefu, zaidi ya miaka 8 iliyopita. Lengo kubwa ni kurahisisha lugha inayoandikwa kuelezea matokeo ya kitafiti ili matokeo hayo yaweze kueleweka kwa wananchi na waweze kuyatumia"

Aliongeza kuwa siku zote watafiti wamekuwa wakiandika matokeo ya kitafiti kwa lugha za kisayansi, hivyo, tumeona  namna pekee nzuri ya kupeleka matokeo ya utafiti kwa wadau wakiwemo wananchi ni kuyaandika matokeo hayo kwa lugha rahisi ni kuwashirikisha waandishi wa habari.

Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Bakari Msangi aliipongeza COSTECH kwa kuwezesha mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa mkoa wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro. Tume hiyo imekwisha fanikiwa kutoa mafunzo hayo katika mikoa 7 inayojumuisha mkoa wa Dar es salaam, Unguja, Mtwara, Tanga, Dodoma, Pemba na jiji la Mwanza na kuwezesha usambazaji wa taarifa za Sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa kupitia vyombo vya habari vikiwemo Luninga, Redio, Blogu na Magazeti.

Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka COSTECH, Dkt. Philbert M. Luhunga (wa tatu kushoto waliokaa), Kaimu Meneja Uhifadhi Taarifa na Uchapishaji kutoka COSTECH, Dkt. Bunini Manyilizu (wa pili kulia waliokaa), Mwezeshaji wa mafunzo Dkt. Bakari Msangi (wa pili kushoto waliokaa), Dkt. Paschal Nade (wa kwanza kushoto waliokaa) Mtafiti kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela – Arusha (NM-AIST), Mwakilishi wa Waandishi wa Habari, Pamela Mollel (wa kwanza kulia waliokaa) katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya uandishi wa habari za sayansi, teknolojia na ubunifu kati ya waandishi wa habari na watafiti Jumanne ya tarehe 15 Machi, 2022 katika Ukumbi  wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Jijini Arusha

Kaimu Meneja Uhifadhi wa Taarifa na Uchapishaji kutoka COSTECH, Dkt. Bunini Manyilizu (aliyesimama) na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka COSTECH, Dkt. Philbert M. Luhunga (aliyeketi) akitoa salamu za utambulisho mbele ya washriki (hawapo pichani) wa warsha ya mafunzo ya uandishi wa habari za sayansi, teknolojia na ubunifu