
MHE. SIMBACHAWENE AFUNGUA MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA
MHE. SIMBACHAWENE AFUNGUA MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amezitaka taasisi zote kutumia mifumo ya TEHAMA na kufungamanishwa na mifumo ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora na kwa haraka zaidi.
Waziri Simbachawene amesema hayo wakati akifungua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025, yanayofanyika kitaifa Jijini Dodoma huku akipongeza ushiriki mkubwa ulioonyeshwa na taasisi hizo.
Amesema mfumo wa Serikali mtandao umeleta mageuzi na mafanikio makubwa ikiwemo kutunza muda na kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Waziri huyo amesema takribani taasisi 185 zimeshajiunga kwenye mifumo na kufungamanishwa na mifumo ya Serikali.
"Taasisi zote ambazo bado hazijajiunga na kwenye mfumo hivyo kutofungamanishwa na mfumo wa Serikali, nazitaka kufanya hivyo haraka,"alisisitiza.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Juma Selemani Mkomi amesema maonesho hayo yana malengo mbalimbali ikiwemo kuwaandaa watumishi wa umma ili kukabiliana na changamoto katika utumishi wa umma ambapo jumla ya wizara 23 na taasisi 101 ikiwemo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) zimeshiriki. Ufunguzi umefanyika tarehe 17 Juni, 2025 katika viwanja wa Chinangali Park.
"Jumla ya taasisi 120 tuliziandikia barua ili ziweze kushiriki katika maonesho hayo,"alisema Katibu Mkuu.
Maadhimisho hayo yameanza Juni 16 na yatahimitishwa Juni 23, 2025, yakiwa yamebeba kauli mbiu isemayo “ Himiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”