TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY
(COSTECH)

News

KAMISHENI YA COSTECH YATEMBELEA UJENZI WA JENGO LA STU LA COSTECH JIJINI DODOMA

KAMISHENI YA COSTECH YATEMBELEA UJENZI WA JENGO LA STU LA COSTECH JIJINI DODOMA

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Profesa John Kondolo, ameongoza ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa jengo  la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STU) la COSTECH jijini Dodoma, ambapo amepongeza hatua kubwa iliyofikiwa na mkandarasi anayejenga jengo hilo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Julai 31, 2025 Jijini Dodoma Profesa Kondolo amesema kuwa wamejiridhisha na maendeleo ya ujenzi ambao umeendana na masharti ya mkataba unaotakiwa kukamilika ifikapo Machi 2026.

“Kiwango na ubora wa kazi tulivyoshuhudia vinatupa matumaini makubwa kwamba jengo hili jipya la STU litakuwa na hadhi ya kitaifa na kimataifa katika kuendeleza sekta za sayansi na teknolojia,” amesema Profesa Kondolo.

Ameeleza kuwa jengo hilo linajengwa kwa umadhubuti na heshima inayostahili taasisi muhimu ya COSTECH, hivyo linaonesha kukidhi viwango vya usanifu wa kisasa na matumizi ya muda mrefu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali takriban shilingi bilioni nane za Kitanzania kupitia mradi wa HEET, ukiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuboresha miundombinu ya utafiti na ubunifu nchini.

Dkt. Nungu amefafanua kuwa jengo hilo litakuwa na kumbi za bunifu, kumbi za mikutano ya wanasayansi, na maabara za kisasa zitakazowezesha wabunifu kuwndeleza bunifu zao kwa ufanisi zaidi.

“Tunategemea pia kuwa na nafasi maalum kwa ajili ya wabunifu kupata huduma za Atamizi (incubation) ili kukuza mawazo na ubunifu mpya,baada ya makao makuu kuhamia Dodoma, nafasi iliyokuwa ikitumika Dar es Salaam itatumika kikamilifu kwa ajili ya huduma hizo,” ameeleza Dkt. Nungu.

Aidha, Dkt. Nungu amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutarahisisha uratibu wa shughuli za kitaifa za utafiti na teknolojia kutokana na uwepo wa miundombinu ya kisasa na mazingira bora ya kazi kwa wataalamu na wabunifu.

Kwa upande wake, Msanifu Majengo wa mradi huo, Benedict Martin, ameeleza kuwa usanifu wa jengo hilo umezingatia vigezo vya kisayansi na kiteknolojia kwa kuhakikisha linaendana na mahitaji ya utafiti na ubunifu wa kisasa.

Martin alisema usanifu huo umejumuisha ofisi za kisasa, kumbi za mafunzo, maeneo ya maonyesho ya teknolojia, na mifumo ya kidigitali itakayorahisisha mawasiliano ya kitaifa na kimataifa kwa COSTECH.

“Tumepanga kila kipengele kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha kuwa linaweza kubeba shughuli zote za COSTECH kwa miongo kadhaa ijayo bila kuhitaji mabadiliko makubwa,” alisema Martin.

Kukamilika kwa jengo la STU kunatarajiwa kuimarisha zaidi nafasi ya Tanzania katika utafiti na maendeleo ya kisayansi, ikileta urahisi kwa wanasayansi, wabunifu na sekta binafsi kushirikiana katika kukuza teknolojia na ubunifu nchini.