Costech yatenga sh bilion 1.29 kwa ajili ya tafiti zilizoshinda.
COSTECH YATENGA SH BILION 1.29 KWA AJILI YA TAFITI ZILIZOSHINDA
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kupitia Serikali na wadau imetoa sh bilioni 1.29, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi tisa ya Utafiti katika sekta ya Afya, Kilimo, Uvuvi na Mifugo pamoja na manunuzi.
Hayo yamebainishwa na mgeni rasmi wa tukio hilo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo, wakati akihitimisha Mafunzo ya watafiti ya siku tatu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema kumekuwa na miradi ya utafiti na ubunifu inayofadhiliwa na Serikali kupitia COSTECH, pamoja na hatua mbalimbali za tathimini ili kubaini miradi ya kimkakati na inayolenga kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
“Serikali inajua umuhimu wa utafiti na itaendelea kuboresha mazingira ya utafiti ikiwemo kutoa ruzuku kwa watafiti ili kuleta tija kwa Taifa".
Profesa Nombo anasema, Serikali imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa kuboresha mazingira ya utafiti na ubunifu nchini kutokana na kuamini kupitia tafiti na ubunifu inasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya Afya, uchumi pamoja na kijamii.
Katibu Mkuu ameongezea kusema, Serikali imeongeza rasilimali fedha na kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuvutia wadau ndani na nje ya nchi kuwekeza katika utafiti na ubunifu, hii ni pamoja kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yamevutiwa na kuongeza washirika wa maendeleo wanaochangia katika shughuli za utafiti na ubunifu nchini.
Aidha, Prof. Nombo amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2019-2022), Serikali imeweza kugharamia jumla ya miradi 49 ya utafiti iliyojumuisha zaidi ya watafiti 235 kutoka Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti na Maendeleo nchini, na imetumia Shilingi bilioni 9.04 kwa Taasisi 11 za Elimu ya Juu na Utafiti ambazo zimewezesha kukarabati na kununua vifaa vya maabara za utafiti na miundombinu mingine.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu, amesema kuwa, hivi karibuni wamepokea mapendekezo ya mradi ya utafiti 92 na baada ya kupitia na jopo la wataalamu miradi saba imefanikiwa kupitishwa na hata hivyo miradi hiyo saba ya utafiti imejikita katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, elimu pamoja na manunuzi.
“Timu ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekaa na watafiti kwa muda wa siku tatu kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kutengeneza mipango kazi ya miradi yao ili iweze kuwa na uhalisia katika utendaji wake” amesema Dkt. Nungu.
Vilevile Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa katika siku hizo tatu watafiti wameweka mikakati ya kutekeleza tafiti ambazo zimefadhiliwa na Serikali kupitia COSTECH, na tumebainisha kuwa kupitia wafadhili mbalimbali katika kipindi cha miaka mitatu Tume imefanikiwa kuleta shilingi bilioni 9 nchini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya utafiti.
Dkt Nungu amesema fedha hizo zimetumika katika kufadhili miradi mbalimbali ya utafiti ya viwanda ikiwemo Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), na kusema kuwa miradi mingine imetekelezwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo Tanzania (SIDO).
Hivyo Dkt. Nungu amemalizia kwa kutoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu vya utafiti ili kuleta mapendekezo ya mradi mpya kwa ajili ya usalama wa chakula, ambapo imelenga kuwapatia ufadhili wakimama wanaofanya tafiti nchini.
Hata hivyo Watafiti walioweza kijishindia tuzo hiyo ni pamoja na wawakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Neema Lymo, ambaye amesema wamekuja na miradi miwili ya utafiti ambayo imelenga kutatua changamoto katika sekta ya mifugo na uvuvi pamoja na kilimo, na kusema kuna changamoto ya magonjwa ambayo yanaathiri mazao, mifugo na kuleta hasara kwa mkulima na mfugaji kwa wakati ikiwemo masoko na mbegu.
Amesema katika kutafuta majibu ya changamoto hizo timu ya SUA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali wameleta mifumo miwili ambayo itakwenda kusaidia kutatua tatizo hilo.
Pia mtafiti huyo ameongezea kuwa mifumo yote miwili inatumia teknolojia ya kisasa ambapo wa kwanza utatusaidia kugundua magonjwa ya kilimo na mifumo kwa wakati, na Mfumo wa pili utasaidia kuwaunganisha wadau mbalimbali ikiwemo wakulima, wafugaji pamoja na watu wa masoko jambo ambalo litakuwa na tija kwa Taifa.
Kwa kumalizia watafiti wengine ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo, Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Daktari Bigwa wa Magonjwa ya Akili Dkt. Innocent Mwambeki, na wengine kutoka taasisi mbalimbali nchini.