Rais Dkt. Samia Kuzindua Mfuko wa Mikopo wa Sh Bilioni 2.3 kwa Bunifu za Vijana
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua mfuko wa mikopo wa Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya bunifu na teknolojia zinazobuniwa na vijana wa Kitanzania. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alithibitisha hili katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu Kongamano la Tisa la Kitaifa na Maonesho ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE), akieleza kuwa uzinduzi huo utafanyika tarehe 2 Desemba 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Zaidi ya watu 1,000 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo, ambalo linaandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Kilele chake kitakuwa tarehe 4 Desemba 2024.
Katika ufunguzi huo, Rais Dkt. Samia pia atakabidhi hundi ya Sh bilioni 6.3 kwa watafiti 19 wanaojihusisha na tafiti za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo miradi ya nishati safi ya kupikia. Aidha, atatoa tuzo maalum kwa wanasayansi na wabunifu ambao kazi zao zimeleta mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ndani na nje ya Tanzania.
Rais Samia pia atapata fursa ya kutembelea maonesho ya STICE ili kujionea matokeo ya tafiti na ubunifu mbalimbali yanayochangia kubadili mfumo wa kiuchumi na kijamii nchini.
Kongamano la mwaka huu lina kauli mbiu isemayo: “Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Katika Kuhimili Changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi na Kuchangia kwenye Uchumi Shindani.” Lengo la kauli mbiu hii ni kuhamasisha matumizi ya bunifu na teknolojia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi wa ushindani na endelevu.
Prof. Mkenda alieleza kuwa, kongamano hili litatoa fursa kwa serikali kupata michango ya kisera na kitaalamu ambayo itawezesha kuimarisha sera na mikakati ya kukuza ushirikiano baina ya taasisi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kukuza sayansi, teknolojia, na ubunifu kama nguzo kuu ya uchumi na maisha bora kwa Watanzania.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, amewataka Watanzania kujitokeza kushiriki kongamano hilo kwa kutoa mawazo yao na kujifunza bunifu mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja watafiti, wabunifu, na wadau wa sekta mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kujadili, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja katika kukuza mchango wa sayansi, teknolojia, na ubunifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.