COSTECH yachangia kuleta Mageuzi ya kiuchumi katika Elimu ya juu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema taasisi za COSTECH, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) zinajukumu muhimu la kusaidia kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia sekta ya elimu ya juu chini ya mradi wa HEET.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kabla ya ruzuku kwa wabunifu ya siku tatu yaliyoanza tarehe 15 hadi 17 Januari, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi Arusha, Dkt. Nungu alieleza kuwa utekelezaji wa jukumu hilo utapimwa kwa mafanikio ya COSTECH katika kushiriki mageuzi hayo.
Dkt. Nungu alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji miongoni mwa wadau ili kuhakikisha malengo ya mradi wa HEET yanafikiwa.
Alieleza pia kuwa vituo vya ubunifu vinapaswa kupewa kipaumbele, kwani vina mchango mkubwa katika maendeleo ya wabunifu na uchumi wa taifa.
Kuhusu hali ya kumbi za bunifu katika vyuo vya elimu ya juu, aliahidi kuhakikisha taarifa za mrejesho ya “due diligence” kwa taasisi tano za elimu ya juu zinawafikia viongozi husika ili zifanyiwe kazi kwa uzito unaostahili.
Aidha, Dkt. Nungu aliwahimiza washiriki kutumia fursa ya mfuko wa kukopesha wabunifu kwa riba nafuu “ Samia Innovation Fund”, ambao ulizinduliwa rasmi Desemba 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, kwa lengo la kusaidia wabunifu kubiasharisha bunifu zao.