TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY
(COSTECH)

News

COSTECH, SUA waja na suluhisho la magonjwa ya mazao mbalimbali

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) pamoja na taasisi zinazojishughulisha na kilimo, wamekuja na mfumo wa teknolojia unaoitwa "KILIMO APP" ambao unafanya utambuzi wa magonjwa kwenye mazao katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.

Mfumo huo uliobuniwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), unakwenda kuwa suluhisho la kuondoa changamoto katika mazao ya Mahindi, Maharage, Muhogo na Mpunga yanayolimwa kwa wingi hapa nchini.

Akielezea maendeleo ya mradi huo katika ziara ya kutembelea Wilaya ya Mkuranga, Februari 19, 2024, Mtafiti Mkuu kutoka SUA Dkt. Michael Mahenge amesema, teknolojia ya KILIMO APP imezinduliwa rasmi Desemba 2023, maalum kwa kugundua magonjwa ya mazao hayo yaliyoainishwa.

Aidha amesema taarifa hizo kuhusu mazao hayo, zinakusanywa kwa kutumia ndege isiotumia rubani ( drone) na simu za mkononi kwa mashamba makubwa na madogo kwa mikoa minne ambayo ni Pwani, Morogoro, Songwe pamoja na Mbeya.

"Lengo la teknolojia hii ni kuwasaidia wadau na wakulima katika mnyororo wa thamani, utambuzi na utabiri wa magonjwa kutokana na hali ya hewa ya kipindi ikiwemo  kupendekeza njia bora za utatuzi wa changamoto hizo" amesema Dkt. Mahenge.
 
Kutokana na hayo, Dkt. Mahenge ameishukuru Serikali kupitia COSTECH kwa mchango wao katika utafiti wa teknolojia hiyo, ambayo inakwenda kuboresha mazao ikiwemo kuongeza kuchangia kipato kwenye sekta ya kilimo itakayoenda sambamba na wakulima kuendesha kilimo chenye tija ambacho kitaleta matokeo chanya kwa taifa.

Kwa upande wake afisa mazao wilayani Mkuranga Bw. Karani Michaeli  ameishukuru  COSTECH na SUA, kutokana na teknolojia ya KILIMO APP ambayo itasaidia sana wilayani humo kwasababu wakulima wengi hawafahamu aina ya magonjwa yanayosumbua mazao yao, hivyo teknolojia hiyo itarahisisha kuleta usahili wa tatizo la mazao kwa haraka. 

Aidha amesema App hiyo pia itawasaidia maafisa mazao kujua changamoto kwa haraka kwasababu ina uwanja mpana wa kujifunza na italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Naye Bi Mwahija Rajabu Mohamed Mkulima wa zao la Muhogo wilayani Mkuranga amesema, kuletwa kwa teknolojia hiyo kutasaidia sana katika utambuzi wa magonjwa unaokumba mazao yao kwa urahisi na haraka hivyo kurahisisha ongezeko la mazao na kukua kwenye soko. 

Pamoja naye  Mkulima wa mazao ya bustani wilayani Mkuranga Bw. Philipo Shenkiawa amehitimisha kwa kusema, upatikanaji wa afisa mazao kwa wakati umekuwa changamoto kwa wakulima jambo lililopelekea upotevu wa mazao mengi katika maeneo mbalimbali.

Amesema  kupitia KILIMO APP  kutaokoa mazao mengi ikiwemo kuwaingizia fedha nyingi ambazo zitawasaidia kujiinua kiuchumi.