
COSTECH KUANZA UJENZI WA JENGO LA STI JIJINI DODOMA
DODOMA: Ujenzi wa jengo la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH), unaanza Machi 26, 2025 baada ya Mkandarasi wa jengo hilo ni TIL Construction Limited kukabidhiwa rasmi eneo la mradi.
Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kutoka COSTECH, Dkt. Aloyce Andrew amesema hayo jijini Dodoma baada ya kukabidhi eneo hilo kwa mkandarasi huyo.
Dkt. Andrew amesema wamekadhi eneo hilo kwa mkandarasi kwa lengo la kuanza ujenzi wa jengo hilo.
"COSTECH ina jengo Dar es Salaam lakini inatarajia kujenga Dodoma kwa ajili ya kurahisisha utoaji huduma kwa wadau wetu.
"Jengo hilo litakuwa na sehemu ya kuhudumia wabunifu, sehemu ya kuatamia kampuni changa, pia sehemu ya kuratibu masuala ya utafiti," amesema.
Amesema ujenzi huo unatarajia kukamilika ndani ya miezi 12 tokea waliposaini mkataba Machi 24, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya MEKON, Benedict Martin amesema wamekuwepo kwa ajili ya kumkabidhi mkandarasi eneo hilo la ujenzi.
" Tumeshirikiana na COSTECH kupata jengo litakalokidhi matakwa yao yote pia tuna uhakika wa mkandarasi tuliyempata amekidhi vigezo na tunaamini mradi utakamilika bila itilafu yoyote," amesema.
Amesema katika zabuni ya ujenzi kulikuwa na washindani 12, lakini TIL imeshinda kutokana na miradi iliyofanya kabla na kukidhi vigezo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ujenzi TIL, Ding Fubing amesema baada ya kukabidhiwa eneo la mradi wanaanza rasmi ujenzi tarehe 26 Machi, 2025
Amesema,"Wategemee tutafanya kazi nzuri tutaimaliza kazi hii ndani ya muda au kabla ya muda. Vyote vitategemeana na ule ushirikiano tutakaokuwa nao pamoja,".
Akizungumza kwa niaba ya COSTECH, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Imanuel Mgonja amesema wapo na mshauri elekezi Kampuni ya MEKON ambaye atakuwa msimamizi wa jengo hilo.
Amesema naye Mkandarasi Kampuni ya TIL ameahidi ataifanya kazi hiyo kwa wakati na ubora unaotakiwa.
"Kwa niaba ya COSTECH tunawashukuru mshauri elekezi na mkandarasi kwa sababu wanaonyesha wana nia ya kufanya kazi kwa ubora unaotakiwa," amesema.