TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY

Watafiti na Waandishi wa Habari Wakutanishwa Pamoja na Kujengewa Uwezo

Published at: Thu, Nov 25, 2021 10:54 AM

Mafunzo hayo yamefanyika kwa kwa siku mbili (2) kuanzia Jumanne ya Septemba 5, 2021 mpaka Jumatano ya Septemba 6, 2021 katika ukumbi wa mikutano ulipo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Jijini Mwanza.

Akihitimisha mafunzo hayo alisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa kuwa yanatoa fursa kwa waandishi wa habari kushiriki kwa wingi katika kusambaza matokeo ya utafiti yaliyoko katika vyuo vikuu na vituo vya utafiti na maendeleo vilivyoko Kanda ya ziwa.

Ngusa aliwasisitiza waandishi kuhakikisha  wanachakata taarifa za matokeo ya utafiti na ubunifu ili yawafikie wananchi katika lugha rahisi na inayoweza kueleweka kwao.

"Kumekuwepo na dhana kwamba watafiti wanatumia lugha ngumu katika kuwasilisha matokeo ya tafiti wanazizifanya.  Nimejulishwa kwamba mafunzo haya yamewezesha watafiti kujikita katika kutumia msamiati rahisi wanapowasilisha matokeo ya tafiti zao. Nawasihi waandishi mtumie lugha rahisi ili

mlengwa wa kutumia matokeo haya, aweze kuyapata bila kigugumizi," alibainisha.

Alihitimisha kwa kuwashukuru Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuratibu mafunzo haya yaliyowezesha kuwakutanisha pande zote mbili ili kuondoa dhana tofauti ambayo huwaathiri wananchi kwa kukosa taarifa sahihi.

" Nawapongeza COSTECH kwa jitihada hizi na naamini zitakuwa na manufaa kwa nyanja tofauti ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda na sekta nyinginezo."

Mafunzo yaliyofanyika kwa waandishi na watafiti kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ni mwendelezo wa mafunzo yaliyowahi kufanyika mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga, Dar es salaam, Dodoma, Singida, Lindi, Mtwara, Unguja na Pemba.