Published at: Thu, Feb 23, 2023 5:22 AM
MAKAMPUNI MACHANGA NA WANAWAKE KUNUFAIKA NA PROGRAMU YA imbeJu
Katika mwendelezo wa kusaidia jitihada za Serikali kukuza ujumuishi wa kiuchumi nchini, Benki ya CRDB imeingia mkataba wa makubaliano na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Tume ya TEHAMA (ICTC) kupitia programu yake ya ‘imbeJu’ iliyojikita katika uwezeshaji wa wanawake na makampuni machanga (Startups).
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema ushirikiano na Taasisi hizi za Serikali utasaidia kufanikisha malengo ya programu kwa kiasi kikubwa kutokana na jinsi uzoefu wa Taasisi hizi katika kuwawezesha vijana wabunifu katika sekta mbalimbali.
“Ili kuifanya programu hii kuwa yenye ufanisi na kufikia walengwa wengi, tumeona ni vyema kutafuta wadau ambao wana mawazo kama yetu yaani “like-minded partners”.
COSTECH na ICTC wamekuwa wakifanya kazi nzuri ambayo inaakisi utayari wa Serikali yetu katika kukuza biashara na mawazo ubunifu, hivyo tunajivunia kwa hatua hii muhimu,” alisema.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Amos Nungu amesema makubaliano waliyoyaingia na Benki ya CRDB yanakwenda kuoanisha imbeJu na programu za taasisi COSTECH zinazochochea ubunifu wa kibiashara ikiwemo MAKISATU jambo litakalosaidia kuchochea kasi ya ukuaji wa biashara changa katika sekta mbalimbali.
Aidha, Benki ya CRDB pia iliutangazia umma kuanzishwa kwa taasisi isiyo ya faida ya “CRDB Bank Foundation” yenye jukumu la kuanzisha na kutekeleza programu bunifu, endelevu, na shirikishi zinazolenga kuleta ustawi wa kijamii, na kiuchumi kama ‘imbeJu’
Hafla ya utiaji Saini mkataba wa makubaliano ya kuwezesha makampuni machanga na Wanawake ilifanyika katika ukumbi wa Johari Rotana tarehe 20 Februari, 2023 jijini Dar Es Salaam.