TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY

COSTECH YAWAPA MBINU WAANDISHI WA HABARI NAMNA YA KUANDIKA HABARI ZA KISAYANSI.

Published at: Tue, Mar 29, 2022 2:01 PM

Kaimu Mkurugenzi Mkuu COSTECH na Kaimu Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa,Dk.Philibert Luhunga akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watafiti  katika semina ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuripoti habari za kisayansi  iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia inayofanyika jijini Arusha.Picha na Happy Lazaro)

 

 

Wakiwa katika picha ya pamoja ni waandishi wa habari pamoja na watafiti mbalimbali kutoka kanda ya kaskazini wakiwa kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya sayansi na teknolojia (COSTECH)picha na Happy Lazaro)
 
************
 
Happy Lazaro,Arusha 
 
 
Arusha.Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania(COSTECH) imewataka waandishi wa habari kuandika habari za sayansi kwa  kutumia lugha rahisi katika matokeo ya tafiti zinazofanywa na watafiti hapa nchini ili ziweze kuwafikia walengwa wakiwemo wananchi ili waweze kufanya maamuzi.
 
 
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH ,Dkt.Philibert Luhunga  ameyasema hayo wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari na watafiti wa Kanda ya Kaskazini yanayofanyika Mkoani Arusha.
 
 
 
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Tume hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweeden yamelenga kuwapa mbinu waandishi wa habari 25 kutoka mikoa ya Arusha ,Manyara na Kilimanjaro ya namna ya kuripoti babari za ubinifu,Sayansi na Teknolojia.
 
 
“Watafiti wamekuwa wakifanya kazi kubwa za kitafiti ambazo zina matokeo mazuri lakini matokeo haya huandikwa kwa lugha ya kisayansi zaidi na kuchapishwa kwenye machapisho ya kimataifa,hivyo tunaomba waandishi waweze kuyatafsiri matokeo haya kwa lugha nyepesi zaidi ili yaweze kutumiwa na jamii,”amesema Dk.Luhunga
 
 
Aidha ,Dk.Luhunga amesema endapo tafiti hizo zikiandikwa kwa lugha rahisi na zikawafikia walengwa wakiwemo wananchi  itawasaidia kufanya maamuzi mbalimbali na katika kutatua changamoto zao za kila siku.
 
 
Naye ,Mratibu wa mafunzo hayo kutoka (COSTECH),Deusidedith Leonard, amesema mafunzo hayo  yatasaidia kuziba pengo  kati ya waandishi wa habari,Wahariri pamoja na watafiti katika kuwasilisha taarifa za Sayansi na Teknolojia kwenye jamii.
 
 
“Mafunzo haya yatatoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kubaini mbinu bora ambazo zitatuwezesha kufikisha  taarifa za Kitafiti kwa lugha rahisi na kutafsiriwa vizuri ili ziweze kuwafikia walengwa wakiwemo watunga sera ,wafanya maamuzi ,wazalisha mali na wananchi kwa ujumla,”amesema Leonard
 
 
 
Kwa upande wake ,Mwezeshaji Mkuu wa mafunzo hayo,Dk.Bakari Msangi amewataka watafiti hao kuandika kwa ufupi machapisho ya tafiti zao ili iweze kumpa nafasi msomaji kusoma kwa urahisi bila kuchoka.
 
 
“Chapisho linapokuwa fupi linamvutia mtu kusoma ,wanadamu wana shughuli nyingi, hawana muda wa kusema wanasoma tuu ,unakuta mtu anafikiria mambo mengi,mimi nawashauri hawa wanaofanya tafiti zao wafanye chapisho fupi linaloweza kusomwa na watu wengi,”amesema Dk.Msangi