TANZANIA COMMISSION FOR SCIENCE AND TECHNOLOGY

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Yawajengea Uwezo Mameneja Usimamizi wa Tafiti Nchini

Published at: Thu, Nov 25, 2021 10:54 AM

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amehitimisha kilele cha mafunzo ya usimamizi wa Tafiti kwa kuwapatia vyeti washiriki wote 14, wanaojumuisha wakufunzi 2 na washiriki 12  kutoka Taasisi za Utafiti nchini.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa kwa siku nne (4) kuanzia Jumatatu ya Oktoba 25, 2021 mpaka Alhamisi ya Oktoba 28, 2021 katika ukumbi wa mikutano ulipo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI - Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Akihitimisha mafunzo hayo, Dkt. Nungu alisisitiza kwa washiriki kuzingatia ujuzi na maarifa waliyoyapata kupitia mafunzo haya, ikiwemo kanuni za usimamizi wa fedha na manunuzi (principle of due diligence) ili zisaidie kuboresha maeneo yao ya kusimamia miradi na kuongeza tija katika Tafiti nchini Tanzania.

 

Aidha, Dkt. Nungu aliwashukuru washiriki kujitokeza na kuongezea kuwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imekuwa ikifanya utaratibu na utamaduni wa kusimamia rasilimali fedha na manunuzi ili kusimimia vyema fedha za utafiti zinazotolewa na Serikali zikilenga kuboresha vipaumbele vya Taifa katika utafiti kwa kuzingatia maeneo ya kimkakati kama vile Kilimo, Afya na Mifugo.

Kwa upande wake, mratibu wa mafunzo haya, Meneja wa Sayansi Mada  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH, Mhandisi, Mashuhuri Mwinyihamisi Mushi aliwashukuru wakufunzi ambao ni Profesa, Hasyo Mukalu kutoka Chuo Kikuu cha Capetown cha Afrika ya Kusini pamoja na Mkufunzi mwandamizi, Ndugu. Rose Mosha kutoka Taasisi ya Sayansi ya Teknolojia na Nelson Mandela - Arusha (NM-AIST).

Mafunzo hayo yamekutanisha   wasimamizi wa tafiti kutoka taasisi13 za Utafiti nchini Tanzania, ikijumuisha Taasisi ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo Tanzania (TEMDO), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Shirika la Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Taasisi ya Utafiti ya Kilimo (TARTARI), Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Zanzibar (ZARI), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), Taasisu ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia  (COSTECH), Taasisi ya Utafiti wa Udhibiti Viuatilifu (TPRI), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) pamoja na Taasisi ya Nyumbu-Kibaha.

Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya washiriki wengine, Dkt.Cecilia China pamoja na Dkt. Asanterabi Lowassa waliipongeza COSTECH kwa kuwapa fursa hii ya kujifunza na kupata ujuzi katika kusimamia changamoto na fursa za utafiti nchini, mbinu za kusimamizi tafiti, namna bora yaa kundaa andiko la miradi shindani pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathmini katika maeneo yetu ya kazi, na mwisho watafiti kuahidi kuwa kupitia uwezeshwaji huu kutoka Tume utasaidia kuongeza kiwango cha usimamizi wa utafiti kitaifa na kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya utafiti katika jamii ya watanzania.