
PROF. MKENDA AZINDUA SAMIA EXTENDED SCHOLARSHIP KWA FANI ZA SAYANSI YA DATA, AKILI UNDE NA SAYANSI SHIRIKISHI VYUO MAHIRI DUNIANI
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amezindua rasmi programu ya Samia Extended Scholarship DS/AI+, inayolenga kufadhili wanafunzi wa Tanzania bara na Zanzibar kusoma katika vyuo vikuu mahiri duniani katika fani za kimkakati za Sayansi ya Data, Akili Unde (Artificial Intelligence), na Sayansi Shirikishi kwa mwaka wa masomo 2025/2027.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Julai 8, 2025 jijini Arusha, Prof. Mkenda alieleza kuwa mpango huo unalenga kuwanufaisha wanafunzi 50 waliobobea katika tahasusi za sayansi asilia zenye hisabati ya juu (advanced mathematics). Alibainisha kuwa waombaji watakaofanikiwa watahitajika kushiriki Kambi ya Kitaifa ya Maarifa kwa muda wa miezi kumi (10) katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kabla ya kuanza masomo yao nje ya nchi.
Prof. Mkenda alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwekeza kwa dhati katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Alitoa wito kwa vijana kutumia fursa hiyo kwa bidii na maarifa ili kuchochea mageuzi ya kisayansi na kiteknolojia nchini.