
SAHARA SPARKS YAADHIMISHA MIAKA 10, YAZIDI KUTAFAKARI MABADILIKO YA SERA
SAHARA SPARKS YAADHIMISHA MIAKA 10, YAZIDI KUTAFAKARI MABADILIKO YA SERA
Dar es Salaam, Jumatano, Julai 16, 2025.
Jukwaa la uongozi wa fikra la Sahara Sparks, linaloongoza kuunda mazingira ya ubunifu, teknolojia na ujasiriamali, linaadhimisha miaka 10 ya mchango wake nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla, huku ikitafakari safari ya muongo mmoja ya kushinikiza mabadiliko ya Sera.
Katika maadhimisho haya, Sahara Sparks inatafakari safari yake ya muongo mmoja ya kushinikiza mabadiliko ya sera, ili kuwezesha kampuni changa (startups), na kuhamasisha jamii kupitia suluhisho za kibunifu.
Akizungumza jijini Dar Es Salaam tarehe 16 Julai, 2025 Mkurugenzi wa Sahara Ventures Jumanne Mtambalike amesema kaulimbiu ya "Mchango Uliotazamwa Upya” (Impact Revisited) ", Sahara Sparks 2025 inatarajiwa kufanyika Septemba 5 na 6 katika Ukumbi wa Mlimani City,uliopo Dar Es Salaam.
Amesema kama sehemu ya maadhimisho haya, siku hiyo kutazinduliwa Ripoti ya Mchango wa Sahara Sparks, nyaraka ya kina inayobeba historia ya mabadiliko na mafanikio ya Sahara Sparks na kampuni mama yake ya Sahara Ventures kwa kipindi cha miaka 10.
Mtambalike amesema ripoti hiyo pia itaangazia mchango wa jukwaa hili katika kukuza ubunifu, teknolojia na ekosistemi ya Kampuni Changa (startup) pamoja na athari halisi katika jamii hasa za ngazi ya chini.
Mkutano huu wa juu utajumuisha mijadala ya uongozi wa fikra yenye lengo la kuchochea mabadiliko ya kimfumo, kuendeleza usaidizi kwa Kampuni Changa (startups) na kuchunguza mustakabali wa ubunifu, teknolojia na ujasiriamali barani Afrika.
Amefafanua kuwa washiriki watakuwa ni wawekezaji, washirika wa maendeleo, wabunifu, wajasiriamali, watunga sera na wasomi kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.
Kwa kuendeleza dhamira yake ya kuwezesha Kampuni Changa (startups), Sahara Sparks 2025 pia itaandaa soko la bidhaa za ubunifu ambapo wajasiriamali wataonesha bidhaa na huduma zao, zaidi ya hapo wabunifu wanaochipukia watapata nafasi ya kuwasilisha mawazo yao mbele ya hadhira.
Hata hivyo kilicho cha thamani zaidi kwetu siyo muda huo tu, bali ni athari tuliyoiacha kwenye ekosistemi ndiyo maana tumelipa jina la kaulimbiu yetu mwaka huu kuwa “ Mchango Uliotazamwa Upya” (Impact Revisited).
Amesema pia katika miezi kadhaa iliyopita, wametafakari kuhusu miradi yetu na athari tulizozisababisha kwa jamii, Kampuni changa (startups) na wabunifu mbalimbali na Matokeo yake hasa ngazi ya jamii za chini ni ya kushangaza na ya kutia moyo sana.
Mtambalike pia alitoa shukrani kwa wadau waliounga mkono safari ya Sahara Sparks kwa miaka yote, wakiwemo mashirika ya maendeleo, taasisi za Serikali (COSTECH), makampuni binafsi na jumuiya pana ya wajasiriamali.
“Safari yetu haingewezekana bila msaada wa washirika wetu wa muda mrefu tunatoa
shukrani za pekee kwa COSTECH, Ubalozi wa Finland hapa Tanzania, Ubalozi wa Uswizi, UNDP Tanzania, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, FSDT na wadau wengine waliotuunga
mkono tangu mwaka 2016,"amesema Mtambalike.
"Ushirikiano wao ulikuwa msingi muhimu katika kuwezesha ndoto yetu kuwa halisi na kuikuza hadi kuwa jukwaa kubwa la ubunifu barani Afrika.”amesema.
Washirika wa mwaka huu ni pamoja na COSTECH, UNFPA, UN Women na TSA, huku wengine wakitarajiwa kujiunga. Washiriki na waoneshaji bidhaa wanaweza kujisajili kupitia tovuti ya saharasparks.com.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amesema COSTECH wamekuwa sehemu ya safari ya Sahara Sparks tangu mwanzo kabisa.
Amesema waliamini katika wazo la awali – kutoa jukwaa kwa mijadala yenye athari katika ekosistemi kama wasimamizi wa sekta ya ubunifu na teknolojia nchini, waliona ni wajibu wao kuiunga mkono, hasa wakati ambapo jukwaa la aina hii halikuwepo.
Hata hivyo amesema kupitia Sahara Sparks, tumeona mabadiliko mengi katika mfumo mzima wa ubunifu, na kwa hilo, tunajivunia kuadhimisha mafanikio haya pamoja nao.