DKT. NUNGU APONGEZA UZALISHAJI BIDHAA KIWANDA CHA SOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt Amos Nungu amekipongeza kiwanda cha Vijana cha Soma kilichopo jijini Mwanza, kinachozalisha bidhaa mbalimbali za vitenge, ngozi, yakiwemo mabegi ya sola kwa kutumia taka.
Dkt. Nungu ametoa pongezi hizo leo Septemba 25, katika ziara fupi ya kutembelea kiwanda hicho, ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana hao.
Dkt. Nungu pamoja na pongezi hizo kwa uongozi wa kiwanda hicho, amewataka Soma kuendelea kuzalisha bidhaa hizo kwa wingi ili kuziuza ndani na nje ya nchi.
"Naomba muendelee kuzalisha kwa wingi bidhaa hizi, ili ziwezwe kuuzwa nje ya nchi," amesema Dkt. Nungu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha Soma Bw. Innocent Sulley amesema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2018 na vijana watano wahitimu wa chuo kutoka Mwanza Tanzania.
Aidha amesema kiwanda hicho kilishiriki Mashindano ya Kitaifa ya Ubunifu (MAKISATU) na kushinda hatimaye kuingia katika programu ya kusaidiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo kiasi cha shilingi 26,500,000/= zilitolewa na Serikali kupitia COSTECH ili kuanzisha kitengo cha ukamilishaji na udhibiti wa viwango vya ubora wa bidhaa zao (Finishing and Quality Control) katika kiwanda hicho.
Bw. Sulley amesema hata hivyo uanzishwaji wa kituo hicho kumesaidia kuboresha thamani na ubora wa bidhaa zao, kwa sasa bidhaa kutoka Soma zipo kwenye majaribio ya awali ili kuingia katika soko la Ulaya hususan Polandi, Uholanzi na Ujerumani.