MAJALIWA: wakuu wa idara na taasisi za umma waombwa
Waziri Mkuu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (mb) amewaambia wakuu wa idara na taasisi za umma kutenga bajeti ili kuimarisha utoaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa wakati siku ya tarehe 27 Machi 2023 alipokuwa akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kikaokazi cha 18 cha maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikali katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kituo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere- JNICC- Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Majaliwa pia ametoa rai kwa maafisa hao kuongeza ubunifu ili kusukuma ajenda za kiserikali pamoja na kuwataka Viongozi wao kuhakikisha wanawashirikisha maafisa Habari na Uhusuiano katika Vikao vya maamuzi ili waweze kutoa taarifa sahihi za utekelezaji wa mipango na miradi ya Serikali pamoja na elimu kwa wananchi wote.
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeshiriki kikao hicho kupitia Maafisa wake ambao wameungana na maafisa wengine zaidi ya 500 kushiriki kikao hicho kilichobeba kauli mbiu isemayo "Mawasiliano ya kimkakati, Injini ya Maendeleo."
Kwa upande wake mwenyeji wa Kikao hicho, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye ameongeza kuwa Wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano kwa Umma (National Communication Strategy), Mkakati wa Mawasiliano wakati wa Majanga (Risk Communication Strategy) pamoja na Mkakati wa Kujitanganza Kitaifa (National Branding Strategy)
Aidha kupitia Kikaokazi hicho Waziri wa Habari amekabidhi Tuzo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini mchango wa Maendeleo ya Sekta ya Habari, demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari nchini.